Thursday, 3 September 2015
KIINGILIO KUITAZAMA TAIFA STARS NA SUPER EAGLES SH 7,000
picha kwa hisani ya bin zubery
MAANDALIZI ya mchezo kati ya Tanzania (Taifa Stars) dhidi ya Nigeria (Super Eagles) yamekamilika, ambapo leo Shirikisho la Mpira wa Miguu nchini (TFF) limetangaza viingilio vya mchezo huo wa jumamosi kati huku kiingilio cha chini kabisa kikiwa shilingi elfu saba tu.
Viingilio vya mchezo huo wa kuwania kufuzu kwa Fainali za Mataifa ya Afrika (AFCON Qaulifier 2017) kundi G itakua ni VIP A Tsh 40,000, VIP B Tsh 30,000, VIP C Tsh15,000, Rangi ya Machungwa (Orange) Tsh 10,000, na viti vya rangi ya Bluu na Kijani Tsh 7,000.
Tiketi za mchezo huo zinatarajiwa kuanza kuuzwa kesho siku ya ijumaa saa 4 kamili asubuhi katika vituo vya Ofisi za TFF - Karume, Buguruni Oilcom, Mbagala Dar Live, Ubungo Oilcom, Makumbusho Stendi, Uwanja wa Taifa, Mwenge Stendi, Kivukoni Feri, Posta Luther House na Big Bon Msimbazi Kariakooo.
TFF inawaomba watanzania, wapenzi na wadau wa mpira wa miguu kununua tiketi za mchezo huo katika magari yaliyopo kwenye vituo vilivyotajwa ili kuondokana na tatizo la kuuziwa tiketi zisizokuwa halali.
Jeshi la Polisi nchini kwa kushirikiana na idara nyingine za kiusalama wameandaa usalama wa kutosha katika kuelekea kwenye mchezo na kuhakikisha kila mpenzi wa mpira wa miguu anaingia kushuhudia mchezo huo salama na kuondoka salama.
Mchezo huo utaanza saa 10:30 jioni kwa saa za Afrika Mashariki utachezeshwa na waamuzi kutoka nchini Rwanda ambao wanatarajiwa kuwasili leo jioni pamoja na kamisaa wa mchezo huo.
Waamuzi wa mchezo huo ni Louis Hakizimana (mwamuzi wa kati) Honore Simba (mwamuzi msaidizi), Jean Bosco Niyitegeka (mwamuzi msaidizi), Abdoul Karim Twagiramukiza (mwamuzi wa akiba) wote kutoka Rwanda na kamisaaa ni Charles Kasembe kutoka nchini Uganda.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment