TIMU
ya Taifa ya Tanzania yenye wachezaji wapatao 30 na viongozi 7 wa
michezo mbalimbali inatarajia kuondoka Jijiji Dar es Salaam kesho jioni
na ndege maalum kuelekea Congo Brazaville kushiriki katika Michezo ya
Afrika (All Africa Games) itakayofunguliwa rasmi Septemba 4, 2015.
Hayo
yamesemwa leo Jijini Dar es Salaam na Mkurugenzi Idara ya Habari, Assah
Mwambene wakati wa Mkutano na Waandishi wa habari kuhusu Timu ya Taifa
itakayoshiriki katika Michezo ya Afrika (All Africa Games) huko Congo
Brazzaville.
Mwambene
amesema kuwa Tanzania itawakilishwa na Michezo sita ikiwemo Mchezo wa
Ngumi za Ridhaa yenye wachezaji watatu, Timu ya Mpira wa Miguu ya
Wanawake (Twiga Stars) yenye wachezaji 18, na Timu ya Riadha yenye
wachezaji wanne.
Nyingine
ni Timu ya kuogelea yenye wachezaji wawili, wachezaji wawili wa Judo
pamoja na Michezo kwa watu wenye Ulemavu yenye wachezaji wawili.
Naye
Mkurugenzi Msaidizi Maendeleo ya Michezo, Juliana Yassoda amesema kuwa
Timu ya Taifa ya Tanzania ilikua iondoke kwenda Congo Brazzaville leo
lakini kutokana na ugumu wa upatikanaji wa nafasi katika ndege
mbalimbali timu hiyo imelazimika kuondoka kesho na usafiri maalum.
Michezo
ya Afrika (All Africa Games) inatarajiwa kuanza kutimua vumbi kesho na
Twiga Stars itafungua dimba na Ivory Coast Septemba 6, kabla ya
kumenyana na Nigeria Septemba 9 na kumaliza mechi za kundi lake kwa
kumenyana na wenyeji Kongo-Brazzavile Septemba 12.
Timu mbili kutoka kundi A zitaungana na timu mbili nyingine kutoka kundi B kucheza hatua ya nusu fainali.
No comments:
Post a Comment